JUMA KATUNDU WA MSONDO NA KARAMA REGESSU WA SIKINDE ‘WAJIUNGA’ NA BABU SEYA …WATASHIRIKI VICKING’S NIGHT JUMAMOSI HII



Waimbaji Juma Katundu wa Msondo Ngoma na Karama Regessu wa Sikinde wamejiunga na Nguza Vicking (Babu Seya) kwaajili ya onyesho maalum lililopewa jina la “Vicking’s Night”.


Hiyo haimaanishi kuwa waimbaji hao wamezihama bendi zao, bali wanakwenda kwa Babu Seya kwaajili ya onyesho hilo litakalofanyika Jumamosi hii katika ukumbi wa King Solomon, jijini Dar es Salaam.

Katundu na Karama ndiyo waimbaji watakaoimba na kuitikia nyimbo za Babu Seya katika onyesho hilo ambalo pia litamshirikisha mtoto wa Nguza, Papii Kocha.

Hili linakuwa onyesho la kwanza la kibiashara kwa Nguza tangu yeye na Papii walipotoka jela kwa msamaha wa Rais Magufuli mwishoni mwa mwaka jana.

Kwa zaidi ya wiki nzima, Karama na Katundu wamekuwa kwenye mazoezi makali ya pamoja na mkongwe huyo kwaajili ya Vicking’s Night.

Saluti5 imebahatika kushuhudia mazoezi hayo ambapo waimbaji hao wameonyesha uwezo mkubwa wa kuimba nyimbo kama “Kalubandika”, “Maria Nyerere”, “Kadiri Kansimba” na nyingine nyingi.

Haijajulikana itakuweje iwapo Nguza atanogewa na waimbaji. Watahama jumla bendi zao au watachomoa? Ni jambo la kusubiri.

Kwasasa hivi onyesho la Vicking’s Night ndiyo habari ya mjini, mamia ya watu wanaisubiri kwa hamu show hiyo yenye kiingilio cha 20,000, 50,000 hadi 1,000,000.

 Nguza na Juma Katundu
 Kutoka kushoto ni Juma Katundu, Nguza Vicking na Karama Regessu wakiwa mazoezini
Juma Katundu, Nguza Vicking na Karama Regessu wakiwa na mdau wa muziki Juma Mbizo



Labels: