KLABU ya Simba imesema
haijafanya mazungumzo na straika wa kimataifa wa Yanga raia wa Zimbabwe, Donald
Ngoma.
Rais wa Simba, Evans Aveva
amekaririwa akisema kwamba jambo hilo ni geni kwake na kama limefanyika basi
itakuwa limefanywa na watu wengine.
Kumekuwa na habari zinazosambaa
kwenye mitandao ya kijamii kwamba Simba imefanya mazungumzo na Ngoma lakini
uongozi wa Simba umekanusha jambo hilo.
Hata hivyo, chanzo kimoja
kimesema kuwa Ngoma amefanya mazungumzo na Simba kwa nia ya kujiunga na timu
hiyo msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika ndani ya Yanga.
“Simba imefanya mazungumzo na
Ngoma na kuonekana kwamba wamekubaliana baadhi ya mambo ambapo kama hali
ikienda vizuri basi msimu ujao atavaa jezi za Simba baada ya mkataba wake
kumalizika ndani ya Yanga,” kilisema chanzo hicho.
Kama usajili huo utakamilika,
basi Ngoma aliyetua nchini miaka miwili iliyopita akitokea FC Platnum ya
nyumbani kwao, atajiunga bure na Simba, huku timu yake ya sasa, yanga ikikosa
fedha za usajili wake kutokana na mkataba wake kumalizika.
Lakini Aveva amesema kwamba yeye
binafsi taarifa hizo hazijamfikia na kama zipo basi labda itakuwa Kamati za
chini yake ndizo zinafahamu kila kitu juu ya jambo hilo.
Kamati ya Usajili ya Simba iko
chini ya mwenyekiti wake, Zakaria hans Poppe pamoja na wajumbe wengine “makini”
na wanasemekana kuweza kufanya lolote kwa wakati wowote.
Labels: SOKA